Jumamosi 24 Oktoba 2026 - 12:38
Madhaifu Kumi ya Marekani, Nguvu Yake ni ya Kioo na Nyumba ya Buibui/  Kipindi cha Subira Kimefikia Hatam

Hawza/ Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Qum amefafanua madhaifu kumi ya Marekani yaliojitokeza waziwazi katika vita vya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa ripota wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A’rafi, katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa ya tarehe 23 Oktoba 2026, iliyofanyika katika Muswalla wa Quds mjini Qum Iran, alisema: “Vita vilivyolazimishwa dhidi ya Iran na mhimili wa Muqawama vilianzishwa na Trump na Netanyahu, ambao ni wachinjaji na wanyongaji wa zama hizi.”

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini Iran  aliendelea kusema: “Dunia nzima inajua kwamba sisi hatukuwa waanzilishi wa vita hivi. Hata wakati walipokuwa kwenye meza ya mazungumzo, walivunja mikataba, wakakanyaga maadili na kusimama dhidi ya Iran, Mapinduzi ya Kiislamu na Umma wa Kiislamu. Vita hivi havikuwa chaguo letu, bali vililazimishwa kwetu.

“Walikuwa wamejiwekea malengo mbalimbali katika vita hivi, yakiwemo kuupigisha magoti Umma wa Kiislamu na taifa la Iran. Hapo awali, hawakuwa wakitangaza waziwazi kwamba walilenga kuipigisha magoti Iran na kuilazimisha kujisalimisha, lakini leo hii wanasema jambo hilo waziwazi.”

Mjumbe wa Baraza la Walinzi wa Katiba Iran, alisema: “Vita hivi vilitokea kwa kuzingatia malengo hayo waliyokuwa wamejiwekea, lakini matokeo yake yaliushangaza ulimwengu mzima. Taifa la Iran na mhimili wa Muqawama vilisimama imara kwa ushujaa mkubwa na kwa kukabiliana na mashambulizi yasiyo na kifani.

“Kwa sasa, imepita zaidi ya miezi minane, lakini malengo yao ya kuishambulia Iran kwa muda wa wiki moja na kuiangamiza hayajatimia. Kinyume chake, kwa zaidi ya usiku 250 sasa, wananchi wetu wameendelea kuwa mitaani, huku wapiganaji wakiwa kwenye mahandaki yao, tayari kuchukua hatua kwa kufuata amri za Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Haya ndiyo matokeo ya vita hivi.”

Alisema: “Marekani, licha ya kuwa na uwezo na rasilimali zake zote, ni kama jumba la kioo na nyumba ya buibui. Tuko katika kipindi muhimu cha kihistoria, na hatuna njia nyingine isipokuwa kusimama imara dhidi ya mnyama huyu mkali na mkatili.”

Kwanza: Chuki dhidi ya Marekani duniani imefikia kiwango kisicho na kifani

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Qum aliongeza kusema: “Wachambuzi wao wenyewe wanakiri kwamba kwa sasa tunashuhudia kushuka kwa kiwango cha mtaji wa kijamii na imani kwa Marekani kusikokuwa na kifani. Chuki dhidi ya Marekani imefikia wastani wa zaidi ya asilimia 60 duniani. Wameendelea kuipoteza heshima yao ambayo tayari hawakuwa nayo, kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko hapo awali.”

Aliendelea kusema: “Hali hii ni nzito sana kwa serikali inayojigamba kwa madai mengi, inapokabiliwa na kiwango hiki cha chuki dhidi yake duniani, hususan katika Ulimwengu wa Kiislamu.”

Pili: Marekani ni dhaifu licha ya kuwa na kila kitu

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini Iran alisema: “Vita hivi vimeonesha kwamba Marekani, licha ya kuwa na vikosi vyake vyote vya majini pamoja na nguvu kubwa za kijeshi na kiintelijensia, ni dhaifu sana na inaweza kuathirika kwa urahisi inapokabiliana na vita visivyo vya kawaida.”

Tatu: Karata mpya za kimkakati dhidi ya Marekani zimejitokeza

Aliongeza kusema: “Kuna karata mpya za kimkakati zilizodhihirika, ambazo Marekani haikuwa imezitambua hapo awali. Miongoni mwake ni Mlango-Bahari wa Hormuz, bei ya mafuta, bei za bidhaa duniani na njia kuu za kiuchumi duniani.

“Marekani imetambua kwamba maeneo haya yanaweza kuathirika kwa urahisi sana, na kwamba Iran pamoja na mhimili wa Muqawama vina uwezo mkubwa katika maeneo hayo.”

Nne: Ushindani wa ndani nchini Marekani na Israel umeongezeka

Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum alisema: “Ushindani wao wa ndani hauna tofauti kwetu, kwa sababu wote wanafanana. Hata hivyo, leo hii ushindani huo wa ndani umeongezeka kwa kiwango kikubwa, na migawanyiko mikali imejitokeza miongoni mwao, tofauti na hali iliyokuwepo kabla ya vita.”

Tano: Orodha ya malengo ya mashambulizi imeongezeka

Alisema: “Orodha ya malengo yao ya mashambulizi ni kubwa zaidi kuliko yale yaliyolengwa katika Vita vya Kumi na Mbili Vilivyolazimishwa na Vita vya Ramadhani.

“Kama hawaamini, basi watakapopata tena ujasiri wa kufanya mashambulizi, wataona jinsi orodha hii ya malengo ilivyo kubwa na yenye utajiri wa maeneo yanayoweza kulengwa. Mabomu ya muda yanayoweza kulipuka wakati wowote yameanza kufanya kazi ndani ya mfumo wenu wenyewe. Kuongezeka kwa orodha ya malengo ya mashambulizi ni matokeo ya uasi wenu katika vita vya hivi karibuni.”

Sita: Enzi ya kushambulia na kukimbia imefikia mwisho

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini Iran alisema: “Leo hii wametambua ukweli wa kauli ya Kiongozi wetu Shahidi, aliposema kwamba enzi ya kushambulia na kukimbia imefikia mwisho. Taifa la Iran na vikosi vyake vya kijeshi vitaendeleza sera hii kwa kufuata amri za Amiri Jeshi Mkuu, na wataendelea kuwapiga mapigo mazito.”

Saba: Kipindi cha subira ya kimkakati ya Iran kimefikia mwisho

Akieleza kwamba kipindi cha subira ya kimkakati na kuzingatia mazingatio ya Iran kimefikia mwisho, alikumbusha: “Kipindi cha kusema kwamba nchi fulani ni jirani yetu na kwa hiyo tunapaswa kuzingatia hali yake kimekwisha. Hatutaendelea tena na sera ya kufanya maridhiano nanyi kwa sababu ya mazingatio hayo.”

Nane: Misingi ya Israel inayokalia ardhi za wengine imetikisika

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Qum alisema: “Utawala wa Israel unaokalia ardhi za wengine, kwa mwonekano wa nje, umepata mafanikio fulani nchini Syria na Ghaza, lakini misingi yake imekuwa dhaifu na yenye kuyumba zaidi. “Utawala huo wa Israel unaokalia ardhi za wengine si nguvu ambayo mnaweza kutegemea kwa ajili ya mustakabali wenu.”

Tisa: Uchumi unaoweza kuathirika kwa urahisi

Alisema: “Uchumi wenu ni mkubwa, lakini unaweza kuathirika kwa urahisi sana. Aidha, mnasababisha madhara kwa uchumi wa nchi nyingine pia, na dunia ina hofu kutokana na udhaifu na uwezekano wa uchumi kuathirika.”

Kumi: Udhalimu wa Marekani dhidi ya dunia umefichuka

Ayatullah A’rafi alisema: “Kiburi na majivuno ya kistaarabu na ya kimfumo ya Marekani, pamoja na dhuluma yake dhidi ya mataifa, vimefichuka zaidi kuliko wakati mwingine wowote. “Kauli za majivuno zinazotolewa na Trump zinaonesha kuporomoka kwa ustaarabu na kupoteza heshima kwa nchi hiyo mbele ya dunia.”

Alikumbusha kwa kusema: “Haya ndiyo madhaifu yenu kumi mapya ambayo mmeipitia na kuijionea katika vita hivi. Leo hii mnatishia, lakini mjue kwamba mkijiingiza katika mapambano mapya, mtajidhuru wenyewe. Taifa hili litaendelea kusimama imara na kutetea heshima na utukufu wake, na hatimaye litawapigisha magoti.”

Mambo muhimu ya kuzingatia

Kwanza: Hatupaswi kuonesha udhaifu mbele ya adui.

Viongozi wanapaswa kuelewa kwamba mbele ya adui, ni lazima waoneshe uwezo, nguvu na msimamo thabiti. Tuko katikati ya mapambano makubwa na katika njia panda kati ya udhalili na heshima. Hatupaswi kumdharau adui; tunapaswa kumfahamu vizuri, lakini hatupaswi kumwogopa, iii ndio kanuni yetu kuu ya kimkakati.

Pili: Hatua zote zinazohitajika zinapaswa kuchukuliwa kwa ajili ya kukabiliana na kila tukio linaloweza kutokea.

Masuala ya uchumi na maisha ya kila siku ya wananchi yanapaswa kuzingatiwa. Hatua zinazochukuliwa zinastahili shukrani, lakini ni lazima mipango na mikakati iimarishwe zaidi ili kumzuia adui asifikirie kufanya jambo lolote baya.

Tatu: Umoja wa taifa na mshikamano mtakatifu vinapaswa kujengwa kuzunguka Iran, Uislamu na utii kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mshikamano, kuungana kwa mitazamo na kuimarishana ni mahitaji ya lazima katika kipindi hiki cha sasa.

Nne: Vikosi vya kijeshi vinapaswa kuwa tayari, lakini wananchi wanapaswa kuendelea kuwa mitaani.

Enyi wananchi wa Iran, mmeendelea kuimulika mitaa kwa nuru yenu na mmeendeleza uwepo wenu humo. Ushiriki huu katika mikusanyiko ya watu, Swala za Ijumaa, kuhifadhi alama na sherehe za kidini, pamoja na kusimama chini ya bendera ya Uislamu kwa ajili ya kulipiza kisasi na kutetea heshima ya Uislamu, utaendelea.

Onyo kwa Serikali ya Azerbaijan kuhusu kuheshimu maadili ya Mwenyezi Mungu

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Qum, katika ujumbe wake wa kuikumbusha Serikali ya Azerbaijan kuhusu wajibu wa kuheshimu maadili ya Mwenyezi Mungu, hususan vazi la Hijabu, alisema: “Ni jambo lisilokubalika kabisa kwa Umma wa Kiislamu na kwa taifa shujaa la Jamhuri ya Azerbaijan kwamba maagizo yanayokwenda kinyume na Sharia takatifu na maadili yanayokubaliwa na wanazuoni wote wa Kiislamu yatolewe, na kisha wananchi wawekwe katika hali ya kuteswa na kunyanyaswa kwa sababu ya maadili hayo.”

Alisema: “Wanazuoni wa Kiislamu wanatarajia kutoka kwa mataifa ya Kiislamu kwamba yahifadhi na kulinda heshima ya maadili ya Mwenyezi Mungu. “Miongoni mwa maadili hayo ni Hijabu, ambayo ni bendera ya usafi na heshima ya mwanamke, pamoja na kuwa alama ya kufaulu na kufikia ufanisi kwa jamii. “Tunatumaini kwamba mkondo huu usio sahihi unaopinga Hijabu utasitishwa. Suala la Hijabu ni la msingi kabisa, na wanawake wote katika Ulimwengu wa Kiislamu wanapaswa kuichukulia kuwa ni alama ya utambulisho wao wa Kiislamu na jambo linalohakikisha saada na mafanikio yao katika maisha ya dunia na Akhera.”

Saudi Arabia na Bahrain acheni kuwafunga wanazuoni na wananchi

Alisema: “Katika baadhi ya nchi za eneo hili, zikiwemo Bahrain na Saudi Arabia, tunashuhudia wanazuoni na vijana wakifungwa jela kwa miaka mingi. “Wingi wa wafungwa hawa nchini Bahrain na Saudi Arabia ni jambo linalowahuzunisha Maraji' wa kidini na wanazuoni wa Kiislamu. “Inatarajiwa kwamba serikali za nchi hizo zitaacha kuendeleza dhuluma hii. Vilevile, tunatarajia kutoka kwa vyombo vya kidiplomasia vya Ulimwengu wa Kiislamu na Iran kuchukua hatua za kuwaweka huru wananchi na wanazuoni walioko katika nchi hizo.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha